Sunday, November 18, 2012

SERENGETI BOYS WASHINDA 1-0 DHIDI YA 'VIJEBA' WA CONGO BRAZAVILLE ... SASA WANUSA FAINALI ZA AFCON KWA VIJANA CHINI YA MIAKA 17 ZITAKAZOFANYIKA MWAKANI MJINI MARRAKECH, MOROCCO

Huyu naye ana miaka 17? Mchezaji Selemani Khamis wa Serenget Boys (kushoto) akijaribu kumpita mchezaji anayeonekana mkuuuuuubwa aitwaye Antoni Mavoungou wa timu ya vijana ya Congo Brazzavile wakati wa mechi yao ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika  kwavijana wenye umri chini ya miaka 17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo Novemba 18, 2012. Licha ya kushinda, Serengeti wako mbioni kuwakatia rufaa Congo kwa kuchezesha 'vijeba
Kiungo Mudathir Abbas wa timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) alifunga bao pekee kwa 'fri-kiki' kali katika dakika ya 15 kuipa timu yake ushindi wa nyumbani wa 1-0 dhidi ya Congo Brazzavile iliyojaa 'vijeba' wenye 'miili jumba' katika mechi yao ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali za vijanza Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwenye Uwanaj wa Taifa jijini Dar es Salaam leo (Nov 18, 2012).

Faulo iliyozaa goli ilitolewa kwa Serengeti na refa Mganda Miiro Nsubuga baada ya Hussein Ibrahim wa Serengeti kuchezewa faulo na beki wa Congo, Mohendik Brel.

Bao hilo lilipatikana dakika mbili tu baada ya kipa Peter Manyika Peter wa Serengeti kukumbushia makali ya enzi za baba yake aliyekuwa akizidakia Yanga na Taifa Stars, kwa kudaka vyema mpira wa kichwa uliopigwa na Ibara Vinny kutoka karibu na lango.

Wageni waliokuwa wamewazidi 'mno' vijana wa Serengeti kutokana na muonekano wao wa 'miili jumba',  walicharuka baada ya goli hilo na kufanya mashambulizi mfululizo huku wakitawala sehemu kubwa ya mchezo huo ambao ni wazi kuwa matokeo yangekuwa vinginevyo kama si uhodari wa Manyika aliyestahili tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ushindi uliiweka Serengeti katika mazingira mazuri ya kuandika historia kwa kufuzu kihalali kwa fainali za Afrika kwa mara ya kwanza ikiwa watafanikiwa walau kuambulia sare katika mechi yao ya marudiano itakayochezwa Brazzavile wiki mbili zijazo.

Serengeti waliwahi kufuzu kwa fainali hizo lakini wakaondolewa baada ya kukutwa na hatia ya kuchezesha wachezaji wenye umri mkubwa, lakini safari hii wamepata mteremko na kunusa fainali zitakazofanyika mwakani nchini Morocco baada ya wapinzani wao wa awali kujitoa na sasa kubakiwa na kazi ya kuitoa Congo tu ili itinge kwa fainali hizo.

Basile Erikiki, kocha wa Congo aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu dakika mbili kabla ya kumalizika kwa kosa la kumbwatukia refa akiwa karibu na mstari wa uwanja, aliipongeza Serengeti kwa kuonyesha ushindani mkali na soka la kasi, lakini akijipa matumaini ya kusonga mbele kwa kudai kuwa vijana wake watajirekebisha kwa kutumia vyema nafasi watakazopata katika mechi ya marudiano tofauti na ilivyokuwa jana.

Ticha wa Serengeti, Jacob Michelsen, amewasifu vijana wake kwa kuibuka na ushindi katika mechi aliyokiri kwamba ilikuwa ngumu kwa kila upande.
"Ila bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kutimiza lengo la kuwatoa wapinzani wetu (Congo) na kusonga mbele," alisema Michelsen.

Vikosi: Peter Manyika, Miza Abdallah, Mohamed Mohamed, Ismail Gambo, Miraji Adam, Mudathir Abbas, Mohamed Haroub, Joseph Lubasha/Dickson Ambundo (dk.60), Hussein Ibrahim, Selemani Bofu/Tumaini Mosha (dk. 76) na Farid Shah.

Congo Brazzavile: Ombandza Mpea, Imouele Ngampio, Mabiala Charlevy, Okombo Francis, IOndongo Bowrgema, Ibara Vinny, Binguila Bardry, Obassi Ngatsongo, Mohendiki Brei, Atoni Mavoungou na Biassadila Arci.  

No comments:

Post a Comment